Wednesday, May 16, 2012

Shule ya msingi Pambalu

ELIMU

Pambalu shule inayoongoza katika kufaulisha Wanafunzi katika Wilaya ya Sengerema.

LICHA ya ubora wao huo, wazazi hufurahi, watoto wao wanapopata mimba kwa lengo la kuwaoza ili wapate fedha MARA nyingi shule zilizoko mijini ndizo zinazofaulisha zaidi wanafunzi kwa ajili ya kuendeleza masomo katika elimu ya sekondari mara baada ya kumaliza elimu ya msingi. 
Katika picha ni baadhi ya wanafunzi wakiwa katika mapumziko
Wananchi wengi wamekuwa wakisikika na hata kusema kuwa wanafunzi wa vijijini hawawezi kufaulu kutokana na mazingira yenyewe kuwa duni mno katika masomo yao.

Na kuna baadhi husikika wakisema kuwa wanafunzi wa kijijini ndiyo wana akili zaidi kuliko wa mjini na pale wanaposhindwa kuchaguliwa kwa ajili ya kuendelea na masoma ya Sekondari wanasema kuwa rushwa ndiyo inayo changia watoto wakijijini kuachwa. Wanasema kuwa wanafunzi wengi wa mijini baba zao wanakuwa na uwezo hivyo hata kama mtoto akifeli basi jina la mtoto wa kijijini linakatwa na linaingizwa jina la mtoto wa mjini.

Na dhana hiyo imekuwa ikiwaingia wazazi wengi wa vijijini na kuona kuwa watoto wao wanaonewa katika uchaguzi wa wanafunzi wa kuendelea na masomo. Lakini kwa upande mmoja au mwingine dhana hiyo inaweza kuwa ni ya kweli au ni kasumba tu iliyojengeka miongoni mwa jamii ya vijijini.

Shule ya Pambalu iliyoko katika Wilaya hii ya Sengerema katika Mkoa wa Mwanza ni moja ya shule iliyoko katika mazingira duni sana ya utoaji wa elimu kwa wanafunzi washuleni hapo.

Licha ya kuwa na mazingira duni na kuwa kijijini lakini matokeo ya shule hiyo yamekuwa ya kushangaza kama si ya kufurahisha kwani moja ya shule katika Wilaya ya Sengerema inayotoa wanafunzi wengi zaidi kwa ajili ya kujiunga na masomo ya Sekondari.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo, Malale Mathias anaielezea hali hiyo kama alivyozungumza na mwandishi wa makala hii katika shule hiyo. Anasema kuwa siri kubwa ya shule hiyo kufaulisha sana wanafunzi ni kutokana na walimu wa shule hiyo walivyo kuwa na mikakati ya kukuza elimu katika Wilaya yao na ushirikiano mkubwa baina ya walimu. Anasema kuwa licha ya walimu wa shule hiyo kuwa na ushirikiano na wanafunzi wao pia wanafunzi wenyewe wamekuwa na mwamko wa elimu hiyo hali inayopelekea wanafunzi hao kufanya vizuri katika kila mtihani. Akizungumzia twakwimu ya shule hiyo kwa kipindi cha mwaka wa 1999 hadi 2001 anasema kuwa jumla ya wanafunzi 240 walichaguliwa kuendelea na masoma ya Sekondari.

Anasema kuwa katika wanafunzi hao Wasichana walikuwa 130 na Wanaume walikuwa 110 na kufanya idadi ya wanafunzi hao kuwa 240 kwa kipindi hicho cha miaka mitatu.

Akizungumzia idadi kubwa ya wasichana katika kufaulu anasema kuwa inatokana na wasichana kupewa kipaumbele katika maksi hivyo wanaume inawalazimu kufanya kazi ya ziada ili kuchaguliwa kutokana na ukweli kuwa maksi zao ni za juu zaidi kulinganisha na wasichana. 
Mandhari ya nje katika shule ya msingi Pambalu kama inavyoonekana kwenye picha hapo juu
Anasema licha ya kuwa na matokea mazuri katika shule hiyo pia kuna tatizo la vyumba vya madarasa kuwa vichache na hivyo kulazimika watoto wengine kukaa chini wakati wa vipindi kama alivyoshuhudi mwandishi.

Licha ya tatizo hilo pia anasema kuwa kuna baadhi ya wazazi wa watoto wanaosoma katika shule hiyo kuwa na tabia ya kufurahia pindi watoto wao wa kike wanapopata ujauzito kwa lengo la kuwaozesha na kupata fedha.

"Tatizo hili kwa shuleni kwetu limekuwa sugu sana kwani kuna baadhi ya wazazi wamekuwa wakifurahia watoto wao kupata ujauzito na kuwaoza ili wapate fedha za matumizi," anasema mwalimu huyo.

Akizungumzia historia ya shule hiyo mwalimu Malale anasema kuwa jina la shule hiyo limetokana na mzee mmoja aliyekuwa akiishi katika eneo hilo la shule, alikuwa akifahamika kwa jila hilo la PAMBALU.

Anasema kuwa shule hiyo ilianzishwa rasmi mnamo Novemba 11 mwaka 1971 chini ya mwalimu Mkuu wa kwanza Silivester Likonge.

"Toka kuanzishwa kwa shule hii kume kuwa na walimu wapatao 13 waliongoza shule hiyo mpaka sasa,"anasema mwalimu huyo.


No comments: