Wednesday, May 16, 2012

Historia ya Wilaya ya Sengerema.

HISTORIA

WILAYA ya Sengerema ni moja ya Wilaya nane zilizounda Mkoa wa Mwanza . Wilaya hii ilizinduliwa rasmi mwaka 1975 baada ya kumegwa kutoka katika wilaya ya Geita.

Wilaya ya Sengerema kwa upande wa kaskazini imepakana na Wilaya ya Ukerewe, kwa upande wa mashariki imepakana na Wilaya ya Nyamagana na Iemela, kwa upande wa magharibi imepakana na Wilaya ya Geita, Kusini imepakana na Wilaya ya Misungwi na Geita.

Wilaya inaeneo la ukubwa wa kilometa za mraba 8,817 kati ya hizo kilometa za mraba 3,335 ni eneo la nchi kavuna kilometa za mraba 5,482 ni eneo la maji ya Ziwa Victoria.Kati ya eneo la nchi kavu kilometa za mraba 2,511 sawa na 75% ni ardhi yenye rutuba inayofaa kwa kilimo na Ufugaji wakati ambapo kilometa za mraba 824 sawa na asilimia 25% ni eneo la misitu ya asili, hifadhi na majabali.  Ni moja ya Wilaya changa nchini chimbuko ni vijiji vinne

KWA ujumla utakapouliza chimbuko la kijiji, Tarafa, Wilaya, Mkoa na hata Nchi fulani utaambiwa kuwa chimbuko la jina la kijiji hicho au Wilaya na hata nchi hiyo ni jina la mtu mmoja ambaye mara nyingi anakuwa tayari ni marehemu, ambaye alikuwa maarufu sana hapo zamani au jina la sehemu hiyo linaweza kuwa ni kutokana na maafa yaliyowahi kuikumba sehemu hiyo.

Hiyo ndiyo hali halisi ya matokeo ya nchi, mkoa, wilaya, tarafa na vijiji, mara nyingi majina hayo yanakuwa ni ishara ya kumkumbuka ya mtu huyo au maafa hayo na mara nyingi inakuwa kama sehemu ya historia kwa watoto wanaozaliwa na kwa watalii katika mkoa huo au nchi hiyo.Mfano mzuri wa mambo hayo ni Wilaya moja

inayojulikana kama Songea, chimbuko halisi la jina la Wilaya hiyo inatokana na Chifu wa kwanza katika Wilaya hiyo katika miaka ya zamani na hadi kuja jina lake kutukuzwa hadi leo hii ni kutokana na ushujaa wake wa kupinga utawala wa mkoloni ambaye alikuwa ni Mjerumani.
Mpaka leo hii ukienda katika Wilaya hiyo ya Songea utapakuta mahali aliponyongewa chifu huyo kwani pametengenezwa na kusafishwa vizuri na kazi hiyo hufanywa na Halmashauri ya Wilaya hiyo pamoja na zana iliyotumika kwa ajili ya kumnyongea chifu huyo na ile ndoano ailiyomyonga kwa kuning’inizwa katika mti mmoja iliopo mpaka leo na mti huo unaheshimika sana pale Songea.

Mji wa Sengerema kama unavyoonekana katika picha Tukirudi katika Wilaya ya Sengerema chimbuko lake ni tofauti kidogo kama ilivyozeleka kuwa ni urithi wa jina la mtu au ni kutokana na maafa yaliyowahi kutokea kwani chimbuko rasmi la Wilaya hii ni Vijiji vinne ambavyo ni Ibisabageni, Nyampulukano, Nyatukara na Mwabaluhi.
Kwa mujibu wa Afisa Ardhi wa Wilaya hii, Athuman Juma pamoja na baadhi ya wazee wa Sengerema ambao hawakuwa tayari kuyaweka majina yao peupe walipozungumza na mwandishi wa makala hii wanasema kuwa chimbuko la Wilaya hii ni kutokana na vijiji hivyo.

Afisa Ardhi huyo anasema kuwa kwa yeye ndiye mpimaji wa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za wakazi wa Wilaya hii ameweza kupata chimbuko halisi la Wilaya hii na jinsi ilivyoanza hadi kuwa Wilaya katika miaka ya 70.

Anasema kuwa katika kipindi hicho cha miaka ya nyuma sehemu za Ibisabageni zilikuwa ni pamoja na maeneo yote ya kuanzia kwenye bwawa la Sengerema na kuelekea katika njia ya Busisi, Sekondari ya Sengerema, Seminnary ya Saint kalori na maeneo ya kusini mwa Mji wa Sengerema pamoja na maeneo yote ya kusini Mashariki mwa Wilaya hii kwa sasa, yote hayo yalikuwa chini ya kijiji cha Isibageni.

Nao wazee hao wanasema kuwa kijiji cha Nyampulukano kilichukua maeneo yote ya mji yaliyobakia, misheni, shule ya Nyampulukano, Sengerema Seminary pamoja na maeneo ya kiwanja cha mnada wa ng’ombe kwa hivi sasa.

Wanasema kuwa kijiji cha Mwabaluhi kilichukua maeneo yote ya Bomani na kuendelea hadi katika maeneo ya kata ya Igalula na kuendelea.Nacho kijiji cha Nyatukara kilichukua maeneo yote ambayo yako mbele ya misheni hadi katika vijiji jirani ambavyo kwa sasa vinajitegemea kuelekea Kamanga kwa mujibu wa wazee hao.

Afisa Ardhi anasema kuwa licha ya mwaka 1985 vijiji vyote hivyo vimeungana na kuwa Wilaya ya Sengerema lakini bado vijiji hivyo vinatumia taratibu za vijiji vyao kwani bado vina mtendaji wa mtaa kama ilivyo kwa vijijini.

Licha ya hilo anasema kuwa tangu ahamie na alivyokuwa anaisikia Wilaya ya Sengerema hajawahi kusikia Wilaya hii ikiwa katika ukosefu wa chakula kwani ina ardhi kubwa na yenye rutuba ambayo hata kama wakazi wote wa Wilaya hii wakagawana sehemu zao ardhi itakuwa imebaki bado kubwa tu.

Anasema kuwa uchumi mkubwa wa Wilaya hii unategemea sana kilimo na uvuvi kutokana na kuzungukwa kwa kiasi kikubwa na ziwa Vicktoria na hivyo wakazi wengi kujikita katika uvuvi.

Kwa mujibu wa wazee wa Wilaya hii wanasema kuwa mji wa Sengerema unapanuka kwa kiasi kikubwa sana na hivyo wanauhakika baada ya miaka mitano Sengerema haitakuwa kama ilivyo sasa kwani itakuwa imeendelea kwa kiasi kikubwa sana ukilinganisha na baadhi ya Wilaya nyingine katika Mkoa wa Mwanza.

Hata hivyo wazee hao wanasema kuwa Wilaya hii haina wakazi wengi sana ambao ni wasukuma kwani wamechanganyika na wakerewe ambao walikosa ardhi katika kisiwa chao na hivyo kuhamia katika Wilaya ya Sengerema, hata hivyo wanasema kuwa licha ya kuwa na wakerewe lakini hakuna mtu anayeweza kutambua hilo kwani kiluga cha kikerewe ni sawa tu na kisukuma kwani wanasikilizana vizuri tu.

“Wasukuma wengi wapo katika kijiji cha Mwabaluhi na Nyachenche na ndiyo wafugaji wakubwa wa ng’ombe ukilinganisha na vijiji vingine vya Sengerema,” wanasema wazee hao.

Hata hivyo Afisa Ardhi anasema kuwa Wilaya hiyo itapanuka kwa kiasi kikubwa kutokana na watu wengi ambao wameshapimiwa sehemu zao za kujenga kutojenga na mara watakapoanza ujenzi wa sehemu zao basi mji huu utapanuka sana.

“Tumepima viwanja Elfu kumi (10,000) kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za kisasa lakini mpaka sasa nyumba zilizojengwa ni elfu nne tu (4,000) hivyo naamini kuwa mara watu watakapo anza kujenga katika viwanja vyao basi mji utapanuka sana tena kwa haraka,” anasema Afisa Ardhi huyo wa Wilaya.

Wilaya ina jimla ya visiwa 39, visiwa 27 vinakaliwa na watu na visiwa 11 ni hifadhi na kambi za uvuvi.

<< Rudi Juu >>

No comments: